LINDA SANA AFYA YAKO…
Katika kitabu cha The everday manifesto Hero kilichoandikwa na Robin Sharma. Kwenye kitabu hichi mwandishi ametushirikisha maeneo manne ya maisha yako ambayo unapaswa kuyapa kupaumbele sana ili uweze kufanya makubwa katika maisha yako…
Maeneo yote haya manne ni muhimu na unapaswa kuyalinda kwa kuyafanyia kazi, kwa ajili ya ubora wa maisha yako unayoishi…
Maeneo hayo ni kama ifuatavyo;
. Akili yako…
Unapaswa kujijengea mtazamo sahihi wa kiakili ili uweze kufanikiwa. Mtazamo chanya na wa uwezekano utakaokusukuma kufanya makubwa…
. Afya ya mwili wako…
Unapaswa kuwa na afya bora ya mwili ili uweze kufanikiwa. Itakuwa vigumu kupambania mafanikio yako ukiwa unaumwa au ukiwa umekufa…
. Hisia zako…
Unapaswa kujenga hisia chanya zinazokupa msukumo wa kufanya zaidi ili kufanikiwa. Hisia chanya za upendo, matumaini na furaha ni muhimu kwa mafanikio. Hisia hasi za hofu, hasira, wivu na chuki unapaswa kukabiliana nazo kwa namna nzuri zaidi ili zisikuangushe au kukurudisha nyuma…
Imani yako…
Unapaswa kujijenga na kujiimarisha kiimani ili uweze kupambana kufanikiwa kwa kuvuka magumu na changamoto mbalimbali unazozipitia. Imani ndiyo inakuwezesha kujitambua na kujisikiliza kisha kuweza kutumia uwezo mkubwa na wa kipekee uliomo ndani yako…
Eneo la afya yako ya mwili ni moja ya maeneo manne muhimu kwa mafanikio yako.
Kuna maeneo matatu muhimu ya kuzingatia ili kuwa na afya bora ya mwili :-
1. Eneo la kwanza ni mazoezi.
Unapaswa kufanya mazoezi kila siku ili kuimarisha afya yako. Mazoezi yanazalisha kemikali zinazoupa mwili nguvu na msukumo wa kupambana zaidi.Pia mazoezi yanaimarisha kinga ya mwili na mtu kuweza kuepuka magonjwa mbalimbali.
Kuna mazoezi ya aina nyingi, lakini makubwa ni ya kukimbia na kunyanyua vitu vizito.
Hayo yanauweka mwili wako katika afya nzuri.
2. Eneo la pili ni ulaji.
Unapaswa kula kwa usahihi ili uweze kuwa na afya bora kwa ajili ya mafanikio yako.
Eneo la ulaji kuna vitu vitatu;
I/. Aina ya vyakula unavyokula, vinapaswa kuwa vyakula halisi na siyo vya viwandani. Kula zaidi mbogamboga na epuka wanga na sukari.
ii/. Kunywa maji mengi kwenye siku yako, yanauweka mwili kwenye hali nzuri.
III/. Kufunga, kuchagua siku ambazo huli au unakaa muda mrefu bila kula kunaufanya mwili wako ujifanyie matengenezo, lakini pia kunakuimarisha kiroho.
3. Eneo la tatu ni mapumziko.
Mwili wako unahitaji mapumziko ya kutosha ili uweze kuwa na ufanisi na mkubwa zaidi katika shughuli zako za kila siku.Huwezi kufanikiwa kwa kufanya kazi usiku na mchana bila kupumzika Kumbuka wewe ni binadamu mwenye mwili ambao huchoka.
Mwili ukishachoka huwezi tena kufanya shughuli zako kwa ufanisi mzuri.Hivyo unapaswa kupumzika ili mwili wako ujenge nguvu mpya na kujiponya pia.
Unapaswa kutenga muda wa kutosha wa kulala kulingana na mahitaji ya mwili wako.
Na pia unapaswa kuwa na mapumziko ya aina nyingine kwenye siku yako, kama kutembea kwenye asili, kusoma kitabu, kufanya mazungumzo na wengine.Kufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko ni chanzo cha uchovu ambao huwa kikwazo kwa mtu kufika kwenye mafanikio makubwa ya maisha yake…
Tenga muda wa kupumzika na uheshimu ili uweze kufanya makubwa zaidi katika maisha yako…
Natumai kuna kitu umejifunza….
TUZIDI KUJIFUNZA NA TUSICHOKE KUJIFUNZA…